Je, Yesu alikuwa ‘Motivational Speaker’?

Maana ya ‘motivational speaker’ ni ‘msemaji ambaye anawatia moyo watu na kuwahamasisha wafikie malengo au makusudi yao kupitia kubadilisha mtazamo wao.
Yesu na wanafunzi wake

Usemi au fikra ‘motivational speaker’ inatoka wapi? Inatokana na nia na roho ya kizazi hiki ambao hawamjui Mungu.

Nyendo au mafundisho haya yalianza miongoni kwa wasioamini hasa kama miaka 40 iliyopita.

Msingi wa mafundisho haya ni ifuatayo: huhitaji mtu mwingine; huhitaji Mungu au dini; wewe mwenyewe kama binadamu tayari unao uwezo ndani yako kubadilisha maisha yako na kutimiza ndoto zako zote na kutekeleza malengo yako yote!

Wasemaji hao wanaahidi watu watafanikiwa katika kila eneo la maisha yao – inategemea na mtazamo na fikra zao tu!

Ni lazima kubadilisha mtazamo wako tu! Kama ukibadilisha mtazamo wako na fikra zako, yote yatawezekana kwako! Kwa maneno hayo wasemaji hao (motivational speakers) wanachochea hisia za watu ili waamini waweze kutekeleza malengo yao!

Wanahubiri maisha ya kujitegemea kabisa! Kwa msingi, wanahubiri wewe ni mungu! Mamilioni wa wasioamini wamefuata ‘injili’ hiyo.

Wasemaji hao wanaandika  ‘Self-help’ vitabu, yaani, ‘Jisaidie Mwenyewe’ vitabu, kama  ‘10 Steps to Success’, ‘Achieve Your Goals’, ‘Change your Destiny by Changing your Attitude.’ (‘Hatua Kumi Kufanikiwa’, ‘Tekeleza Malengo Yako’, ‘Badilisha Maisha Yako Kupitia Kubadilisha Mtazamo Wako’ nk.)

Bila aibu yo yote, wahubiri wa kikristo siku hizi wanatumia maneno haya haya na lugha hiyo hiyo! Wahubiri hao wanaigia wasemaji wale wasioamini (motivational speakers) kabisa na kupitia mafundisho hayo wanataka kuwavuta vijana wengi sana, na wanafanya hivyo!

Hasa vijana wa kikristo huvutwa na mafundisho hayo na wanakunywa udanganyifu huo kwa sababu yanaahidi mafanikio na matekelezo ya malengo yao!

Kwenye Facebook unaweza kuona wengi hufurahia udanganyifu huo. Kwenye somo hili nataka kuweka wazi kwamba katika Biblia hakuna ‘motivational speakers’ – hata mmoja! Biblia inasema,

“…mtu mmoja alimwambia, ‘Nitakufuata ko kote utakakokwenda.’ Bwana Yesu hakujibu, ‘Oh! Nafurahi unapenda kunifuata. Hongera! Kumbe, unavyo vipaji vizuri nami nitakutumia na utafanikiwa!’ Bwana Yesu akamjibu kwa namna hiyo, “Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake.” (Luka 9:57,58).

Je, unafikiri jibu hili la Yesu lilimpendeza yule aliyejitolea? Je, maneno haya yalimtia moyo? Kwa maneno haya Bwana Yesu alitaka kumuamsha mtu huyo aelewe kwa dhati maana ya ‘kumfuata Yesu’!

Mtu anaweza kuwa na hamu kumfuata Yesu bila kuelewa maana yake, bila ‘kuhesabu gharama’! Labda mtu huyo aliamini Injili ni Injili ya ‘baraka’, yaani, labda akasema moyoni kwake, ‘Ahh, Mungu atanisaidia sasa, atanibariki, ataniokoa kutoka katika mazingira yangu mabaya na atayafanya maisha yangu yawe nzuri na atanisaidia kufanikiwa!’

Jibu la Yesu liliuzima moto wa hamu ya namna hiyo; liliizima hamu yenye tabia ya kibinadamu kujifaidia! Hapana! Injili sio jambo la kujiendeleza mimi mwenyewe, kujifurahisha matelekezo ya malengo yangu, kuboresha ‘uwezo’ wangu, kujitajirisha!

Labda yule aliyetaka kujitolea kumfuata Yesu alifikiri, “Kumbe, ninavyo vipaji, ninao uwezo mzuri ambazo Mungu angeweza kuzitumia kujenga mfalme wake duniani!” Au hudhani hivyo?

Lakini nilisoma kwenye Facebook mtu fulani (mkristo?) aliyeweka post ifuatayo kwenye group ya kikristo fulani, “Mungu anautumaini uwezo wako, basi wewe pia unaweza kufanya vile vile.” Na watu wengi (wakristo?) waligonga ‘like’!

Tunaongea, tunaandika kama Biblia haipo! Watu hawajali neno la Mungu kabisa! Paulo alitanganza, “Sisi wenyewe tulikuwa na hukumu ya mauti katika nafsi zetu ili TUSIJITUMAINIE NAFSI ZETU, bali TUMTUMAINI MUNGU.” (2 Wakor.1:9), na tena, “Maana sisi tu tohara, tumwabuduo Mungu kwa Roho, na kuona fahari juu ya Kristo Yesu, wala hatuutumainii mwili (yaani, uwezo wangu mwenyewe).” (Wafil. 3:3).

Wengi wanatangaza, ‘Usikate tamaa! Usikate tamaa! Utafanikiwa. Songa mbele tu! Mungu atakusaida kufanikiwa!’ Kwa nini wanasema mara nyingi ‘kufanikiwa’? Ina maana ya namna gani?

Kufanikiwa katika biashara yangu? Kwa nini hawatumii lugha ya Biblia? Kwa nini watu hawa hawaandiki ‘Amini Mungu naye atakusaidia kushinda dhambi’ au ‘Usikate tamaa!

Songa mbele na utaona Mungu ni Mwaminifu!’ Kwa nini wengi wanapenda na wanapendelea kutumia lugha ya ‘mafanikio’. Katika muktadha huo, Bwana Yesu hakutumia lugha hiyo wala mitume wake.

Bwana Yesu hatafuti watu wajitoleao. Anatafuta watu ambao watatubu kwa ndani sana, kujikana wenyewe na kuchukua msalaba wao. Mungu anatazamia sisi tuyatafute mapenzi Yake tu, na siyo kuyajenga mapenzi yetu mweyewe kadiri tunavyopenda.

“Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, ‘Nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu.’ (Luka 9:61). ‘Nitakufuata …lakini kwanza…’. Hamna ‘lakini kwanza’, hamna ‘lakini’. Yesu ni Mwana wa Mungu! Huwezi kubadili na Mungu. Yesu hakufa kustarehesha maisha yetu! “Yesu akamwambia, ‘Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.’” (Luka 9:62).


CHANZO: somabiblia

Post a Comment

0 Comments