Kanisa ni nini?




Kwanza kabisa neno Kanisa linamaanisha "mkusanyiko wa waamini" kama ule wa Waisraeli chini ya Musa kwenye mlima Sinai walipopewa Amri za Mungu.

Neno hilohilo lilitumiwa na Wakristo wa kwanza kwa ajili yao wenyewe kusema wameshika nafasi ya Israeli kama taifa la Mungu hata wasipokuwa Wayahudi bali watu wa mataifa mengine.

Jina hilo lilitumika kwa jumuia mama ya Yerusalemu, kwa kila mojawapo ya jumuia za Kikristo zilizotokana na umisionari wa wafuasi wa Yesu Kristo, na kwa umoja wao wa kimataifa uliotazamwa na Mtume Paulo kuwa Mwili wa Kristo, ukiwa na Yesu kama kichwa chake.

Kanisa kama jengo

Wakristo walipoanza kujenga mahali pa ibada, pakaja kuitwa vilevile "kanisa" kwa sababu ndani yake lilikusanyika Kanisa hai.

Hivyo mara nyingi neno hilo linatumika kwa maana ya jengo, ambalo ni mfano mwingine uliotumiwa na Paulo kuhusu umoja wa Wakristo, ukiwa na Yesu kama jiwe kuu la msingi.

Majengo hayo ya ibada yanaweza kuwa na ubora tofauti hata upande wa sanaa; baadhi yake yanatembelewa na watalii na kuhifadhiwa kwa bidii kwa sababu hiyo.

Kwa namna ya pekee ni muhimu Kanisa kuu la kila jimbo (dayosisi), halafu Basilika na Patakatifu.

Madhehebu

Baada ya umoja wa Wakristo kuanza kuvunjika, kwa kawaida madhehebu yaliyotokea yaliendelea kujiita makanisa, ingawa kwa maana mbalimbali: hasa Kanisa Katoliki na Waorthodoksi wanadai kuwa la kwao ndilo linaloendeleza Kanisa pekee la kweli; kumbe Waprotestanti hawatii maanani sana umoja wa Wakristo upande wa miundo, bali ule wa kiroho.

Ndani ya Kanisa Katoliki, linalokubali uongozi wa Papa wa Roma, neno Kanisa linatumika pia kumaanisha kila jimbo na makundi ya majimbo yanayochanga mapokeo yaleyale upande wa teolojia, liturujia, maisha ya kiroho, sheria n.k.

Kwa msingi huo Kanisa la Kilatini, ambalo lilienea kwanza upande wa magharibi wa Dola la Roma (Kanisa la Magharibi), linatofautishwa na Makanisa ya Mashariki yaliyoenea kwanza upande wa mashariki wa dola hilo na nje ya mipaka yake.

Post a Comment

0 Comments