Bishop David Oyedepo, mwanzilishi wa Winners Chapel International


Septemba 27, 1954 alizaliwa Mhubiri wa Neno la Mungu, Mwandishi wa vitabu vya Kikristo, Mfanyabiashara, Mhandisi wa ujenzi na mwanzilishi wa Kanisa la Faith Tabernacle lililopo Ota katika jimbo la Ogun nchini Nigeria na mwanzilishi wa Huduma ya Living Faith Worldwide maarufu Winners Chapel International Bishop David Oyedepo.  

Alizaliwa mjini Osogbo nchini Nigeria. Jina lake halisi ni David Olaniyi Oyedepo. Oyedepo alikulia katika familia ya kidini. Baba yake alikuwa mwislamu, mama yake aliyefahamika Dorcas alikuwa muumini wa kanisa la Holy Order of Cherubim and Seraphim Movement tawi la Aladura huko nchini Nigeria. Oyedepo alikulia kwa bibi yake mjini Osogbo ambaye alimfundisha mambo mengi kuhusu Mungu. Oyedepo aliokoka mwaka 1969 wakati huo akiwa na miaka 15 kutokana na msukumo alioupata kutoka kwa mwalimu wake aliyefahamika kwa jina la Betty Lasher. Alisomea masomo ya Usanifu wa Majengo katika Chuo cha Kwara State Polytechnic. Pia aliwahi kufanya kazi katika Wizara ya Nyumba mjini Ilorin kabla ya kuacha na kuendelea na wito wake wa kimisheni. Alipata shahada ya uzamivu nchini Marekani katika Chuo Kikuu cha Honolulu, Hawaii. Oyedepo aliwahi kusema alipokea upako na maono kutoka kwa Mungu ambaye alizungumza naye kwa saa 18 mnamo Mei 1981. Maono hayo yalikuwa kwa ajili ya watu wanaokandamizwa na Ibilisi. Maono hayo ndiyo yaliyosababisha kuanzishwa kwa huduma ya Winners Chapels International. Mnamo mwaka 2011 Jarida la Forbes lilimtaja Oyedepo kuwa ni Mchungaji mwenye Utajiri mkubwa nchini Nigeria. Oyedepo amekuwa akitoa huduma kupitia Winners Chapel zaidi ya miji 300 duniani kote ambapo barani Afrika yupo katika nchi 45. Pia ameenda hadi Dubai, Uingereza na Marekani. Mbali ya kuwa ni mtumishi wa Bwana kwa sasa ni Kansela katika Chuo Kikuu cha Covenant na Landmark vilivyopo nchini Nigeria.

Post a Comment

0 Comments