MVINYO ULIANZA MIAKA 6000 HATA KABLA YA YESU



SHAMPENI ni mvinyo, hivyo wakati watu wanatarajia kusherehekea Sikukuu ya Krismasi au Noel, na pia sikukuu ya kuupokea Mwaka Mpya wa 2013; ni dhahiri wengi watatumia aina kadhaa za mvinyo huu.

Mvinyo huu hutengenezwa kutokana na zabibu. Kawaida kinywaji hicho huwa ‘cheupe’ chenye ladha tofauti kulingana na matakwa ya watengenezaji. Vile vile kipo katika aina ya White-dry champagne isiyo na utamu wa ladha ya matunda, bali huwa ‘kavu’.

Red champagne huwa na rangi nyekundu, si tamu sana na si chungu. Sweet Champagne ina ladha tamu ya matunda, Non-Alcoholic Champagne haina kilevi ndani yake, bali ni tamu ya kuridhisha, Sparkling Wine ni mvinyo usio wa jina asilia la shampeni ila unafanana na hata unapofunguliwa unalipuka kama shampeni.

Kinywaji hiki kina matumizi ya aina tatu, kwanza ni maalumu kwenye tafrija au sherehe mahususi.

Pili, kinywaji maalumu kitumikacho wakati wa kula chakula au mara baada ya kula. Mvinyo unaotumika hapa ni ule mwekundu ambao ni mzito na mtamu kiasi.

Inaaminika kitaalamu ya kuwa, mvinyo huburudisha na pia husaidia kulainisha chakula tayari kwa kusagwa na kufyonzwa mwilini. Tatu, mvinyo ni kama kinywaji kingine chochote.
Pamoja na kusaidia kulainisha chakula, inasadikiwa pia kuwa mvinyo kiasi husaidia sana mzunguko wa damu mwilini, na husaidia kupunguza mafuta mwilini (lehemu), hivyo kumfanya mtu asiweze kupata shinikizo la damu kwa urahisi.

Asili ya mvinyo huu maalumu ni huko katika bara la Ulaya, na hasa katika nchi ya Ufaransa, ingawaje nchi kadhaa za Ulaya zinazalisha zabibu na kutengeneza mvinyo wa aina mbalimbali.

Msimamizi mmoja wa idara ya vinywaji katika jumba moja la kifalme huko Ulaya, alifahamisha juu ya kuwepo kwa kinywaji ambacho kitatoa shamirisho ya sherehe. Hii ilikuwa mwaka 1742, ingawa mvinyo kutokana na simulizi kadhaa ulianza kutumika yapata miaka 6000 kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo, kwani watawala mbalimbali walimiliki mashamba ya mizabibu, na ndio walikuwa wakinywa kinywaji hicho wakiwa wamejipumzisha.

Zabibu huchachushwa na kutoa mvinyo, wakati mwingine vitu kama vitunguu saumu na hata mchuzi wa samaki viliongezwa kuleta ladha zaidi. Hili lilifanywa zaidi na Warumi wa kale. Inasadikika na kukubalika kuwa mvinyo ni kinywaji chenye heshima na ustaarabu kwa wanywaji wake.

Inaaminika kuna aina 362 tofauti za mvinyo katika nchi kama Ufaransa ambayo ndio hasa mahiri katika utengenezaji wa mvinyo na katika hizo pia kuna aina nyingine zaidi ya 100 ndani yake.

Kiwango cha ulevi katika mvinyo hutofautiana, iko kati ya asilimia 8 hadi 14 ya kilevi, bali aina ya shampeni huwa na kilevi cha asilimia 15 na 24.

Mvinyo si kinywaji cha kunywa mpaka ulewe, ni kinywaji cha hamu tu, watu wengi wanaamini kuwa hakina kilevi.

Kijiji kilichoko kaskazini mashariki ya Ufaransa kinachoitwa ‘Rem Champagne’ ndicho kilichofanikiwa kutoa mvinyo ulio bora na kuamua kuupa mvinyo huo jina la kijiji chao.

Kwa hiyo Champagne ni jina la kijiji kilichotoa mvinyo uliokuwa bora na halisi wakati ule.
Julai 1743, Malkia wa Ufaransa wakati huo ndiye aliyezindua shampeni hiyo na tokea wakati huo kinywaji hicho kimetawazwa rasmi ili kiwe kinywaji cha shamirisho kwenye dhifa maalumu au sherehe mahususi, na hapa unaweza kutumia shampeni ya aina yoyote.

Kwa mantiki hiyo basi, ni dhahiri kinywaji hicho cha shampeni hufunguliwa na kunywewa mwanzo tu wa sherehe husika inapofunguliwa rasmi kwa hotuba ili kuipa baraka stahiki.
Waalikwa au wahusika wa sherehe hiyo (maharusi, wahitimu au wali na wengine) hutiliwa kinywaji hicho kwenye glasi zao kiasi tu; kisha wote husimama wakiwa wameinua juu glasi zao, na watu wote kwa pamoja hupiga ukelele mara tatu wakisema ‘Chiaz’ (cheers au cheer-up!) kugonganisha glasi zao, na kunywa huwa ni kwa funda moja kinywaji chote.

Shampeni inayofunguliwa kwenye sherehe inapendeza inapofunguliwa ipige ‘mshindo’ na ikirusha ‘povu jeupe’ juu. Ili kufanikisha tukio hili, shampeni isiwekwe kwenye jokofu kwani itapata baridi sana na kutolipuka.

Shampeni inayotumika kama kinywaji kingine cha kawaida huwa haihitajiki kulipuka na kurusha povu juu; kwa mfano mko hotelini kwenye meza na wateja wengine hamtakiwi kuwamwagia shampeni yenu.

Unashauriwa kuilaza kwa muda mrefu chupa yenye kinywaji kabla ya kuifungua, ili kile kizibo chake kiwe kimelowa kwa ndani, na hii itarahisisha ufunguzi wake; kizibo kinapokuwa kikavu mno mara nyingi hugoma kufunguka ama kukatika kabisa.

Na ukiishatoa ule waya ulioifungia chupa hiyo, anza kusukuma kizibo kwa kidole gumba huku unaizungusha chupa na hapo itafunguka kwa mshindo kama inavyokusudiwa.

Kutokana na ukavu wa kizibo kwa ndani ya chupa, na watu wengi kutokujua ‘siri hiyo’ ya ufunguaji wake; wengi wao wanakataa kushiriki ufunguzi wa chupa ya shampeni wakiogopa kuadhirika isipofunguka.

Maharusi kuwanywesha makungwi wao kwa nia ya kuwashukuru kwa ajili ya kuwasimamia, tendo hilo sio sahihi kabisa kwani hiyo sio shampeni ya shukurani kwao.

MC ni vema ukifanya udadisi katika mbinu zako zote, kabla ya kuamua kujitosa kwenye ‘mic’ na kutangaza au kuwaomba waalikwa washiriki kwenye tukio fulani.

Inawezekana kabisa kinywaji hiki kikatumika mwisho wa shughuli. Je, ni shughuli za namna gani hizo?

Hizi ni shughuli ambazo mwisho wake ndio panapofikia tamati ya shughuli yenyewe; kwa mfano mwisho wa mashindano, kwani pale anapotangazwa mshindi kama kipo kinywaji hicho, basi hufunguliwa na kurushwa kwa wingi na hata wahusika kumwagiana kwa furaha.
Nawatakia heri ya Sikukuu ya Krisimasi na Mwaka Mpya.

Post a Comment

Previous Post Next Post