TB Joshua is no more

 

TB Joshua (1963-2021)

TB Joshua, mhubiri wa Kimataifa raia wa Nigeria alifariki dunia usiku wa kuamkia Juni 5, 2021. Jina lake halisi ni Temitope Balogun Joshua, alizaliwa Juni 12, 1963. Amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 57.

Alikuwa mwinjilisti, mchungaji na mtoaji wa hisani katika jamii. Huyu ndiye mwanzilishi wa huduma ya SCOAN (The Synagogue, Church of All Nations). Alikuwa akifanya huduma yake kupitia Emmanuel TV yenye makao yake makuu jijini Lagos, Nigeria. Ni miongoni mwa watumishi wa Mungu wachache ambao ni mamilionea  katika zama za sasa, inathibitishwa hivyo kutokana na kuwa na uwezo wa kusafiri kwa kutumia ndege yake binafsi.

TB Joshua alikuwa maarufu barani Afrika na nje ya mipaka hadi Amerika huku akipata uungwaji mkono kwa kiasi kikubwa katika mitandao ya kijamii hususani Facebook, pia You tube na Emmanuel TV. Alijichotea umaarufu mkubwa kama Mchungaji Maarufu katika You Tube. Enzi za uhai wake alitunukiwa tuzo mbalimbali ikiwamo ile ya OFR ambayo hutolewa na serikali ya Nigeria kwa watu wake ambao wamekuwa na msaada kwa jamii chini ya Sheria ya Na. 5 ya mwaka 1964 ya Tuzo za Kitaifa. Tuzo hiyo aliipokea mnamo mwaka 2008.

Jarida la The African Report na New African Magazine yanamchukuliwa kuwa ni miongoni kati ya Waafrika 50 bora wenye ushawishi katika bara la Afrika. Kulingana na Jarida la Forbes, mnamo mwaka 2011 TB Joshua alitajwa kuwa mchungaji wa tatu kwa utajiri duniani licha ya kukana taarifa hiyo.

TB Joshua alikuwa akifahamika kwa kuibua sintofahamu, hatua ambayo mnamo mwaka 2010 serikali ya Cameroon ilimfungia kuingia nchini humo. Nchini Tanzania aliweka miguu yake mnamo mwaka 2015 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wakati wa utawala wa Jakaya Mrisho Kikwete.

TB Joshua alipokelewa na Dkt. John P. Magufuli ambaye walikuwa na ukaribu wa kifamilia kwa miaka mingi. Mchungaji huyo alikaribishwa katika Ikulu ya Tanzania na kuzungumza na Rais wa Awamu ya nne Mheshimiwa Kikwete kisha kuzungumza na Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mnamo mwaka 2015 Edward N. Lowassa.

TB Joshua alizaliwa katika mji wa Arigidi Akoko, Kaskazini Magharibi ya Jimbo la Ondo nchini Nigeria. Alipewa jina la Balogun Francis wakati akisoma katika shule ya Kikristo ya Madhehebu ya Anglikana ya St. Stephen kati ya mwaka 1971 na 1977 huku akishindwa kumalizia mwaka mmoja katika elimu yake ya sekondari.

Kuzaliwa kwake kunazungumzwa katika biography yake kuwa kulizungukwa na matukio mengi ikiwamo ya kukaa tumboni mwa mama yake kwa miezi 15 kisha siku saba baada ya kuzaliwa kwake alinusurika kifo baada ya jabali kuanguka juu ya nyumba yao.

Juni 2019 TB Joshua alizuru mji wa Nazareth ambako kulikuwa makazi ya Yesu Kristo na kukaa huko kwa siku mbili. Tukio hilo lilivuta vyombo vya habari duniani kote licha ya kuzungukwa na vikwazo vingi ikiwamo viongozi  wa dini kuwahamasisha waumini wao kugomea ziara hiyo katika mji huyo.

Takwimu za Forbes zilikadiria kuwa TB Joshua alikuwa akitumia kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 20 kwa ajili ya programu za elimu, afya na rehabilitation kwa ajili ya Wanajeshi wa zamani wa Niger Delta , pia wezi wa kutumia silaha walioamua kuachana na kazi hiyo na wafanyakazi wa ngono ambao waliamua kutubu na kuanza maisha mapya.

Post a Comment

0 Comments