Shabaha ya kuitafsiri Biblia katika lugha mbalimbali


1. Shabaha ya maelezo: watu wazidi kuelewana maana ya Maandiko Matakatifu, Yambidi kila Mkristo kujisomea kwa taratibu Neno la Mungu na kulitafakari. Lakini baadhi ya vitabu vya Biblia ni vigumu; vyataka maelezo. Lakini maelezo hayo kusudi lake si kuiondoa haja ya kuyatafakari maneno ya Biblia bali kuwa kama mtu asindikizaye mgeni kuanza safari yake sawasawa na baadaye kumwacha aendelee mbele peke yake.

Makusudi Matatu: Msaada utakiwao hasa nao wasomao Biblia mara ya kwanza ni wa namna tatu, ndizo hizi:

a) Kueleza kwa nini vitabu viliandikwa na wakati gani. Vitabu ni vya namna mbalimbali wala havikupangwa katika orodha ya kuandikwa. Kuna vitabu vya mafunuo, vya historia, vya mashairi n. k. na vingine nusu hivi, nusu hivi. Basi yafaa kujua kabla ya kusoma kitabu hiki ni cha namna gani, kiliandikwa kwa kusudi gani, na wakati gani. Hayo yaelezwa katika utangulizi wa kila kitabu.

b) Kueleza jinsi vitabu vya Agano la Kale viwianavyo na Agano Jipya. Ingawa vitabu ni mbalimbali hueleza jambo moja, Mungu alivyo. Kwetu sisi. Wakristo Agano la Kale hakina maana pasipo Agano Jipya. Kusudi lote la Agano la Kale ni kuuweka tayari ulimwengu na hasa taifa teule la Wayahudi kwa kuja kwake Kristo. Tena ni vigumu kuelewa vizuri Agano Jipya tusiposoma Agano la Kale na kuona kwa nini Yesu alizaliwa kuwa Myahudi. Wayahudi peke yao walijaliwa mafunuo safi ya Mungu wa kweli na kwa hiyo baadhi yao walikuwa

Tayari kumpokea Masiya aliyetabiriwa alipotokea. Basi, tusipoelezwa hatutafahamu maana ya ndani ya mengi yamhusuyo Kristo.

c) Kuchota mafundisho yatuhusuyo sisi. Ingawa nyakati na mambo ya nje ni mbalimbali, lakini Mungu ni yeye yule wala habadiliki (Yak. 1:17), basi twaweza kugundua mafundisho ya kutufaa sisi katika mambo ya Mungu na watu.

3. Umoja wa Biblia: Basi mtu angeweza kuuliza kwa nini twajumlisha maandiko mbalimbali namna hii katika kitabu kikubwa kimoja, ndicho Biblia. Jibu lake ni ya kuwa maandiko yote hueleza habari za Mungu, jinsi alivyoumba vyote, jinsi ashughulikavyo na wanadamu, kuwabariki, kuwaongoza, kuwarudi, hata kutukomboa na dhambi zilizotusonga tangu zamani za Adamu wa kwanza kwa kutupelekea Adamu wa pili, ndiye Mwokozi wetu.

4. Mwangaza wa Mungu: Waandishi wa Biblia waliongozwa na Roho Mtakatifu, yaani Roho Mtakatifu aliwaongoza ili wafahamu sawasawa habari za Mungu ambazo alitaka kuwafundisha watu kwa maandiko ya Biblia. Halafu Roho Mtakatifu aliongoza waandishi waandike habari zake namna ilivyofaa; siyo kusema kwamba waliandikishwa kila neno kama kwa imla. Twaweza kuueleza ukweli fulani kwa maneno mbalimbali na kwa mifano mbalimbali. Waandishi walichagua kwa uhuru maneno na mifano. Lakini ingawa hivyo Roho Mtakatifu aliwaongoza ili waandike habari za Mungu sawasawa walivyofahamishwa naye moyoni. Twaita uongozi huo wa Roho Mtakatifu mintarafu waandishi wa Biblia karama ya "mwangaza".

5. Kusoma Biblia katika Umoja na Kanisa lote: Roho Mtakatifu husema nasi katika Maandiko Matakatifu. Lakini angalia, hata Shetani aweza kutudanganya kwa maneno ya Biblia, kama alivyojaribu kumtega Kristo nyikani kwa kutaja: "Atakuagizia malaika zake; na mikononi mwao watakuchu-kua; usje ukajikwaa mguu wako katika jiwe" (Mt. 4:6 kutoka Zab. 91 : 11-12)

Kwa hiyo tukiona mawazo yetu yanapingana na mafundisho ya Kanisa tusithubutu zaidi na wengine wote wamekosa. Twaweza kudhani kwamba sisi tumesikia kufahamu Maandiko Matakatifu tu tukiyasoma katika Umoja wa Kanisa lote.

6. Taratibu ya kuisoma Biblia: Basi ni wajibu wetu, tena ni furaha yetu, kuisoma Biblia kwa taratibu na kwa heshima. Bora kutumia kawaida hii:

a) Tuweke nafasi kila siku, robo saa au zaidi kama tulivyo na nafasi, kujisomea aya chache na kuzitafakari. Tusijaribu kusoma nyingi na kwa haraka haraka, maana hatutafaidiwa zaidi; ni afadhali kusoma kidogo mara mbili tatu na kutafuta maana ya ndani.

b) Tusali kwanza huku tukiomba msaada wa Roho Mtakatifu tuelewe na masomo yetu na kujaliwa kusikia sauti yake. Tutunge sala wenyewe au tukiona bora tutumie sala hii au nyingineyo:

Kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Amina. Ee Mungu uliwafundisha mioyo yao wenye imani kwa nuru ya Roho Mtakatifu; Utujalie kwa Roho huyo tuyajue mambo yote kwa akili; na kuifurahia sikuzote faraja yake takatifu. Kwa Bwana wetu Yesu Kristo Mwana wako; Aishiye na kumiliki pamoja nawe, katika umoja wake Yeye huyo Roho Mtakatifu, Mungu daima milele na milele. Amina.

Lakini kwa vyovyote tusali sala hii ya uzatiti kwa uangalifu mwingi, huku tukiomba msaada wa Mungu kwa moyo.

c), Tusome aya chache na kuzitafakari aya zote kwa uangalifu. Waweza kutumia maelezo chini ya ukurasa na utangulizi wa kila kitabu ili kupata msaada wa kuyaanzisha mawazo yako; lakini usitegemee misaada hiyo ya nje tu bali jaribu kupata mawazo yako mwenyewe kutoka kwa Roho Mtakatifu; hivyo utamtolea Mungu sadaka ya akili zako ulizokirimiwa naye. Yafaa kujihoji, "Je aya hizi zanifundisha nini?"

d) Mwishowe, kaza nia ya kushika shauri la Mungu uliojaliwa na kumshukuru kwa nafasi hii ya kujisomea (kumbuka jinsi wengi wasivyoweza kusoma, wengine hawana Biblia, wengine hawajasikia bado Injili, na kuwaombea). Weka Biblia mahali pa salama, isiliwe na wadudu wala kuchafuka kwa njia yoyote.


mcrctv@gmail.com







Previous Post Next Post