Na Ezekiel Kamanga, Mbeya
.Kutoka kushoto ni Askofu Dk. Nicodemus Nyenye akiingia na Askofu Asumwisye Mwaisabila
Kutoka kushoto ni Askofu Nyenye, Askofu Mwaisabila (katikati).
Askofu Mwaisabila akimshukuru Mchungaji Asajigwe Mwaisabila aliyemwongoza sala ya toba mwaka 1957
Akizungumza katika Ibada Maalumu ya kumshukuru Mungu na kumpongeza Askofu Askofu Asumwisye Mwaisabila wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God(EAGT), Gilgali Mwanjelwa, Jijini Mbeya kwa kutunukiwa shahada mbili za heshima katika Uzamivu , Askofu Dk. Nicodemus Nyenye wa Kanisa hilo Makao Makuu Dar es Salaam alisema anamfahamu vizuri Askofu Mwaisabila tangu anaanza utumishi wake na kupata shahada hiyo ni haki yake kwani amepita katika mapito mengi na magumu.
“Ninamfahamu vizuri kwani katika utumishi wake alifiwa na watoto 6 kati ya 11 aliowazaa, ndugu walimshauri aende kwa waganga wa kienyeji kupata ufumbuzi kwa hakikuwa kitu cha kawaida katika ukoo wao, lakini alivumilia na kuzidi kusonga mbele na huduma hii, pia mwaka 1977 alikuja Dar es Salaam pale Temeke nikiwa mshirika kuhubiri kanisa aisee nilibarikiwa na huduma yake” alisema Askofu Dk. Nyenye.
Askofu Dk. Nyenye aliendelea kusema kama si uaminifu mbele za Mungu hata sasa wasingekuwa wanamjua Askofu Mwaisabila katika huduma ya kumtumikia Mungu, hivyo aliwataka watumishi wa Mungu wanaongoza makanisa(wachungaji) kuwa waamnifu hata ukamilifu wa dahari.
Pia Askofu Dk. Nyenye aliwapongeza washirika wa Kanisa hilo kwa mshikamano waliouonyesha tangu Askofu Mwaisabila ameanza huduma yake Mwanjelwa Jijini humo.
“Nichukue nafasi hii tena kuwapongezeni washirika wa kanisa hili kwa mshikamano wenu mliouonyesha kwa kumtunza Askofu Mwaisabila ambaye ametunukiwa shahada yake ya Uzamivu kwani bila ninyi hakika asingeweza peke yake”. Alisema Askofu Dk. Nyenye.
Kwa upande wake Askofu Mwaisabila aliwashukuru watu walioshirikiana naye hadi kupata shahada hizo, siri kubwa ya mafanikio hayo ni kunyenyekea chini ya mkono wa Bwana Mungu.
“Tangu nimeanza huduma ya uchungaji mwaka 1959 kama shemasi na baadaye Mtumshi Mtenda Kazi, nimepita katika mapito mengi ambayo asingekuwa Yesu nisingeweza kufika hapa nilipo, lakini kunyenyekea kwangu mbele za Mungu ndiko kulikofanya haya yote”. alisema Askofu Mwaisabila.
Askofu Mwaisabila aliendelea kusema hatamsahau mtu wa kwanza kumuongoza sala ya toba mwaka 1957 Mchungaji Asajigwe Mwaisabila(89) ambaye alikuwepo katika sherehe hizo kwani wakati huo Mungu alimtumia kumwonyesha njia mpya iliyomfanya afike hapo.
Hata hivyo aliwashauri watumishi wa Mungu kuendelea kunyenyekea kwa Bwana Yesu ili awakweze kwa wakati wake kwani wengine hutaka kufanikiwa harakaharaka hali ambayo huwafanya wamkosee Mungu.
Askofu Mwaisabila alizaliwa mwaka 1935 katika kijiji cha Ndala, Mwakaleli wilayani Rungwe Mkoani Mbeya, alitunukiwa shahada mbili za heshima za udaktari (uzamivu), Honorary Doctor Degree in Divinity na Honorary Doctor Degree of Philosophy in Leadership na Chuo Kikuu cha Omega Global cha nchini Afrika Kusini Februari 26 mwaka huu.