FGBF MBEYA: KUNA WACHUNGAJI WALIOINGILIA TAALUMA

JANUARI 31, 2012, Majira ya Alasiri nikiwa katika shughuli zangu simu inaita na haikuwa na jina lolote isipokuwa namba; bila ya hofu napokea na sauti ya mtu aliyenipigia inasikika masikioni mwangu kuwa nahitajika na Askofu Kingdom Mwaijande wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowiship Jimbo la Mbeya.
 ASKOFU KINGDOM MWAIJANDE
Nachukua hatua ya kuanza safari kuelekea Kabwe Jijini Mbeya mahali liliko kanisa hilo nikitokea Soko Matola kwa mabasi madogo maarufu nchini Tanzania kama “daladala” na wakati mwingine “Vipanya”.

Ilinichukua muda wa dakika 20 kufika mahali lilipo kanisa hilo na siku hiyo kulikuwa na hali ya mawingu na mvua za rashasha huku kila mmoja akiendelea na shughuli zake, kabla sijafika mbele ya kanisa naagaza kwa mbali na kukutana na trekta la kutengeneza barabara maarufu kama “greda” ama “kijiko” likiendelea na kukwetua barabara kama ilivyo kwa msimu wa 2011/2012 Halmashauri ya Jiji la Mbeya imepanga kukarabati barabara zilizo kwenye halmashauri hiyo.

Hebu tuachane na hilo, naona kibao cha kanisa hilo kikiwa na maneno FGBF Jimbo la Mbeya nakutana na aliyeniupigia simu na kujitambulisha kwa jina la Nzenga. Na kuniongoza kuelekea Ofisini kwa Mchungaji na Askofu Mwaijande.

Ofisini kwake mara baada ya Salamu na kutakia hali anaanza kunipa makusudi makuu a kuniita Ofisini kwake na kusema ukweli ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuingia katika ofisini kwake.

Askofu Kingdom Mwaijande anaanza kwa kuorodhesha mambo ambayo atazungumza nami (Jabir Johnson)
  • Ukristo na Mbinguni
  • Makanisa na Roho Mtakatifu
  • Kanisa na Dunia
  • Ubatizo wa Maji
  • Wachungaji na Maaskofu
UKRISTO NA MBINGUNI
ASKOFU KINGDOM MWAIJANDE AKIWA OFISINI KWAKE
Askofu Mwaijande anaanza kwa kunukuru maneno ya Mungu kutoka Kitabu cha Yohana 14:6
“Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli , na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi”.
Pia alinikuru katika kitabu cha Mathayo 3:2
“Tubuni kwa kuwa ufalme wa mbinguni umekaribia”.

Akaeleza kwa kirefu sana kuhusu suala la Ukristo unavyomwelekeza mtu kwenda mbinguni na kwamba kweli ya Neno ya Mungu itamweka mtu mbali na dhambi hatimaye uzima wa milele.

Pia alisema Mbinguni ni kuzuri, na kuongeza kuwa ni nchi iliyo bora Waebrania 11:13-16, Ufunuo 21:23-27

KANISA NA ROHO MTAKATIFU
Askofu Mwaijande akasema kanisa la sasa haliishi kwa kumtegemea Roho Mtakatifu hivyo limekuwa likienda bila kujua uelekeo ni wapi hasa ukizingatia Roho Mtakatifu ndiyo dira ya Kanisa

Pia aliongeza kusema Upentekoste sio mdomoni ni matendo na kwamba badala ya kujifunza wakristo wamekuwa wakienda makanisa  kupoteza muda hali inayosababisha Roho Mtakatifu kulikimbia kanisa.

KANISA NA DUNIA
Askofu Kingdom Mwaijande alizungumzia jinsi kanisa lilipofikia kwa sasa kuwa dunia imehamia kanisani, hivyo badala ya watu wa mataif wajifunze kutoka kanisani, kanisa limekuwa likiiga kutoka huko na kuyaingiza.

Akanukuru kitabu cha Warumi 12 na kusema kuwa Biblia imewataka waamini kutoifuatisha dunia namna inavyooenda na kuhoji kuwa “ Je tutaweza kufika mbinguni kama tunavyotaka”. Na kuongeza kwamba sio kazi nyepesi.

Pia alinukuru maandiko ya Neno la Mungu kutoka kitabu cha Kumbukumbu la Torati 1:35- na kusema kwa sasa dhambi imekithiri ulimwenguni na kwamba Mungu hana mchezo na hilo. 

UBATIZO WA MAJI.
Askofu Kingdom Mwaijande akasema imefikia hatua makanisa yameanza kutoutilia manani ubatizo wa maji mengi kama hatu muhimu sana katika kufika mbinguni.

Aliongeza kusema kama watu wanataka kuiona Mbingu basi ni lazima wafanye kile Yesu alichokifanya kwani Yesu hakuwa mjinga na kwamba hakuona maji sehemu nyingine ya Israel zaidi ya Mto Jordan na kwenda kubatizwa huko.

WACHUNGAJI NA MAASKOFU
Katika suala hilo Askofu Mwaijande alilizungumzia kwa uchungu mwingi na kusema kweli ya Neno la Mungu imepotezwa kutokana na wengine kuingilia taaluma.
Alinukuru maandiko mengi lakini kwa uchache ni haya
Yohana 8:31-34
Mithali 14:12
1Tim.2:4
Isaya 9:16
Marko 7:6-9 mstari wa 7 “Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho, Yaliyo maagizo ya wanadamu”.

Hatimaye aliwataka wachungaji na maaskofu wa makanisani kurudi katika mstari na kuacha kufundisha mawazo yao huku waamini hao wakitumbukia kabisa dhambini.

HISTORIA KWA UFUPI YA ASKOFU KINGDOM MWAIJANDE
Alianza kazi ya uchungaji mwaka 1993 akiwa na FGBF jijini Mbeya. Alianza na Kanisa katika Shule ya Msingi Azimio Jijini humo; na mwaka 1998 walihamia Kabwe-Mwanjelwa lilipo mahali hapo kwa sasa. Kanisa la FGBF Kabwe Mbeya lina zaidi ya waamini 500.

Mtayarishaji/Mhariri: Jabir Johnson


Post a Comment

Previous Post Next Post