JAMII ya Wakristo Zanzibar imetakiwa kuwa
watiifu kwa Serikali na kujenga tabia ya kusameheana, ikiwa ni hatua muhimu
katika kufuata mafundisho ya kiongozi mkuu wa dini hiyo, Yesu Kristo.
Akizungumza
na waumini na wafuasi wa dini ya Kikristo katika Kanisa Kuu la Dole Wilaya ya
Magharibi, Unguja, Mchungaji Issaya Simon alisema njia nzuri na pekee ya kuishi
duniani vizuri ni kufuata sheria za nchi na kujenga tabia ya kuvumiliana na
kusameheana kwa matukio mbali mbali.
Amesema
hiyo ndiyo njia ya kweli ya kufanya mawasiliano na Bwana Mungu kama alivyofanya
Yesu Kristo, wakati alipopata matatizo mbalimbali na kwamba muda wote alikuwa
karibu na mola wake.
Ametoa
mfano wa wana wa Israel walivyoishi katika maisha ya tabu na kuhangaika miaka
kwa miaka, lakini walipoamua kumfuata Mungu na kiongozi wake, walifanikiwa
kuondokana na vikwazo na mateso ya Farao pamoja na kuokoka na utumwa.
Waumini
wa dini ya Kikristo walifurika kwa wingi katika Kanisa la Dole ambako walifanya
ibada pamoja na maombi kwa watu wenye matatizo mbalimbali, ikiwemo wagonjwa.
Wakristo
visiwani hapa jana waliungana na wenzao duniani kote kukumbuka siku ya kuzaliwa
kwa mwokozi wao, Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita huko Bethlehem
katika Mamlaka ya Palestina.
0 Comments