WACHUNGAJI wa Kanisa
la Tanzania Assemblies of
God wametakiwa kuacha kuyafanya makanisa wanayoyachunga kuwa ya kisiasa ili
kutunza amani na utulivu katika nchi ya Tanzania.
Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God Dk. Barnabas
Mtokambali aliyasema hayo wakati akiliweka wakfu jengo jipya la kuabudia la
kimataifa la Calvary Christian Centre la Kanisa hilo katika mji mdogo wa Tunduma mkoani Mbeya
Jumatano ya wiki hii.
Akizungumza kwa msisitizo mkubwa Askofu Mtokambali alisema changamoto
iliyopo sasa katika nchi ya Tanzania
na kanisa kwa ujumla ni kwamba mfumo wa vyama vingi umewashika sana watanzania huku
kanisa likiwa katika mpango mkakati.
Askofu Mtokambali katika suala la mfumo wa vyama vingi
nchini Tanzania,
alisema mchungaji akiegemea katika chama fulani atasababisha amani na utulivu
kupotea kwani migongano ya kimaslahi itaingia ndani ya mioyo ya waamini na
makundi ndani ya kanisa yatajitokeza hali itakayomfukuza Roho Mtakatifu.
Suala la Mpango mkakati Askofu Mtokambali alisema utaingia
doa endapo ndani ya kanisa wachungaji watakuwa wakivutia chama fulani na
waliotakiwa kuokoka hawataokoka na mchungaji atatumika kama
kizuizi cha watu kusababisha Injili isisonge mbele.
“Wachungaji miongoni katika kanisa letu wamejiingiza katika
siasa hali ambayo imeleta magomvi na kupoteza ladha ya kuitwa kanisa la Mungu,
hebu fikiria mchungaji anakuwa wa CUF, ama CCM ama CHADEMA au chama chochote
cha siasa nchini ikitokea timbwili nini kitatokea baina ya chama chake na
vingine ambavyo ndani yake kuna washirika ndani ya kanisa analolichunga”
alisema Askofu Mtokambali.
Askofu Mtokambali aliongeza kusema Kanisa la TAG limetoa
ruhusa kwa mchungaji yeyote anayetaka kujiingiza katika siasa lakini kwa
masharti ya kuachana na kazi ya uchungaji
na kuingia katika siasa.
“ Bila hata fujo mchungaji anaruhusiwa kuja kwa wakuu na
kurudisha joho la uchungaji pamoja na kanisa na kwa amani zote tunamwombea ili
afanikiwe katika siasa kama ni ubunge au nafasi yoyote ile katika siasa kuliko
kufanyia siasa kanisani kwani kanisa haliko kwa ajili ya hayo” alisisitiza
Askofu Mtokambali.
Pia alisema Kanisa sio mahali pa kufanyia mambo ya hovyo
yenye kupunguza uwepo wa Mungu, na kwamba Mchungaji yupo kama
mwamuzi baina ya washirika inapotokea kutokuelewana na pia kuwaongeza ufahamu waamini
kuhusu ufalme wa Mungu.
“Mchungaji ni kama mwamuzi uwanjani anapocheza mechi ili
kuweka usawa, hivyo mchungaji anatumiwa na Mungu kuweka usawa ndani ya kanisa
na kuwanidhamisha wale wanaoleta fujo, hata hivyo Sheria za nchi ya Tanzania
hazimruhusu Mchungaji kuwa shabiki wa chama chochote cha siasa” aliongeza Dr.
Mtokambali.
Hata hivyo Askofu Mtokambali aliwataka waumini wa makanisa
yote ya TAG kuishi maisha ya Utakatifu ili Mungu ainuliwe katika mpango mkakati
wa miaka 10 ambao ifikapo mwaka 2018 kanisa liwe na waamini million mbili.
“Maisha ya utakatifu miujiza huja yenyewe, watu huokoka
wenyewe kila kitu hufanyika kwasababu Roho Mtakatifu anakuwa pamoja na
waaminifu wake” alisisitiza
Katika uzinduzi huo Askofu Barnabas Mtokambali alipokelewa
na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi Mheshimiwa Gabriel Kimolo ambaye aliwasisitizia
waamini wa wilaya hiyo waliokuwepo hapo kuwa wilaya hiyo itaendelea kwasababu
ya wacha Mungu.
“ Kama ujuavyo Mbozi imekuwa mahiri sana kwa vitendo vya aibu visivyompendeza
Mungu vya mauaji, ushirikina, uchunaji ngozi na kadhalika lakini kuzinduliwa
kwa jingo hili kutasaidia watu kumjua Mungu wa kweli na kumrudia yeye” alisema
Mheshimiwa Kimolo.
Mchungaji Eliud Kalinga wa Kanisa hilo alisema ataendelea
kuwa mwaminifu wa Mungu na kwa Tanzania Assemblies of God kuhakikisha mpango
mkakati wa 2009-2018 (Decade of Harvest) unatimia na kuzidi pamoja na watu wa
Mungu.
Katika uzinduzi huo kiasi cha milioni 8.5 zilikusanywa
zikiwemo ahadi kwa ajili ya kumalizia jengo hilo kwa upande wa madirisha, kwani kiasi cha
milioni 16 zinahitajika kukamilisha ujenzi wa madirisha.
Pia kila mshirika alishiriki uwekaji wakfu wa jingo hilo kwa maombi ambayo
Askofu Mtokambali aliyaongoza katika ibada hiyo iliyoanza majira ya saa 5:30
asubuhi hadi jioni ya siku hiyo na kuhudhuriwa na watu wa kila dini kutoka
maeneo mbalimbali mkoani Mbeya.
Aidha Askofu, Dk. Barnabas Mtokambali alisindikizwa na
uongozi wa Jimbo la Kusini Magharibi akiwemo Mlezi Askofu Mwaisabila ambapo
kabla ya hapo walikuwa na mazungumzo na mkuu wa wilaya katika ofisi zake katika
mji wa Vwawa yakiwa na madhumuni ya kufahamiana zaidi kwani ni mara yake ya
kwanza kukutana na Mheshimiwa Gabriel Kimolo.
Katika ziara mkoani
Mbeya, Askofu Mtokambali alitembelea pia maeneo ya Nkanga wilayani Chunya,
Mwakaleli- Tukuyu wilayani Rungwe.
Imeandikwa na Johnson Jabir Desemba 14, 2011