MAASKOFU NA WACHUNGAJI WATAKIWA KUSIMAMIA WITO WALIOITIWA

Maaskofu na Wachungaji wa makanisa nchini wametakiwa kuwa waaminifu katika wito walioitiwa kufuatia baadhi ya viongozi wa dini kuhusishwa na kashfa mbalimbali ikiwemo wizi wa mabilioni ya pesa katika akaunti za Tegeta ESCROW na IPTL.

Akizungumza katika Kongamano la Waimbaji wa Makanisa ya Kikristo mkoani Kilimanjaro lililoandaliwa na Kanisa la Pentekoste (FPCT) Mchungaji  James Thomas Ruta alisema uaminifu katika wito wa kichungaji katika kulitunza kanisa la Mungu ni muhimu kuliko chochote.

“Baadhi ya viongozi wa dini wamehusishwa na kashfa mbalimbali lakini ya hivi karibuni ni hii ya IPTL na ESCROW, hii inashangaza sana, kwani maudhui ya kuwa mtumishi wa Bwana ni kuisaidia jamii ikae kwenye mstari, sasa hapa hakuna hicho.” alisema Mchungaji Ruta 

Mchungaji Ruta aliongeza kusema kuwa tamaa ya mali imekuwa kubwa kupita kiasi hali mabayo inasababisha baadhi ya walioko kwenye mamlaka kujinufaisha wenyewe badala ya kulitazama taifa la Tanzania.

“Tanzania ina changamoto lukuki, ikiwemo ukosefu wa vifaa tiba katika hospitali zetu, maji ndio usiseme lakini hapo hapo unasikia mabailioni ya fedha yamechotwa na watu baadhi ambao wanakaa na kujijali wenyewe huku raia wakifa bila kupatiwa msaada wowote hii ni mbaya sana.” aliongeza mchungaji huyo.

Aidha Mchungaji huyo alisisitiza kuwa taifa la Tanzania linahitaji nguvu za Mungu ili liweze kukaa katika mstari ulionyoka, bila hivyo raia wake wataendelea kupoteza maisha kutokana na hali mbaya za kiuchumi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Waimbaji wa Nyimbo za Injili mkoani hapa Frank Kaziri alisema kongamano hilo liliandaliwa kwa ajili ya kuwaleta pamoja waimbaji wa nyimbo za injili mkoani humo, pamoja na kukuza vipaji vyao.

Pia Kaziri aliongeza kusema uimbaji ni huduma  ambayo ikishikiliwa vizuri inaweza kuliponya taifa kutokana na maudhui yaliyomo katika tungo za nyimbo hivyo Mwenyezi Mungu kusikia kilio cha jamii husika.

Hata hivyo Mwanzilishi wa  Umoja huo Jobiso Shemndolwa alisema limeendelea kukaa katika maudhui tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011 na kuiomba serikali ikaze uzi katika kuweka udhibiti wa kazi za wasanii nchini.

Post a Comment

0 Comments