Na Johnson Jabir
MBEYA-TZ
Magazeti ya dini ya Kikristo hapa nchini ya Nyakati, Utatu na Jibu la Maisha yataanza kusomwa hewani katika kituo cha Redio MbeyaFM mwishoni mwa mwezi huu.
Akizungumza kutoka Jijini Dar es Salaam kwa njia ya simu na Wafanyakazi wa Redio MbeyaFM Imani Kajula alisema ni vizuri kila kitu kinapofanyika katika redio kifuate maoni ya wasikilizaji wake.
Aliongeza kusema wengi huanzisha vitu pasipo kufanya tafiti na hujikuta wakiangukia pua na kile kitu walichoanzisha kutoendelea kabisa, hivyo yeye huheshimu sana watu wanaofanya tafiti katika vitu mbalimbali maana huja na majibu yaliyo sahihi.
Pia alisema mkoa wa Mbeya ni mkoa wa Wakristo hivyo ni vizuri wakapata ladha zinazoendana na mambo wanayoyafanya ikiwemo kupata habari mbalimbali kuhusu Mungu kupitia Magazeti ya Kikristo ya hapa nchini.
Hayo yamekuja kufuatia utafiti na ubunifu wa wanahabari wa Redio MbeyaFM kuona mbali namna gani watawafikia wasikilizaji wake, hivyo kipindi cha NURU ya JUMAPILI ambacho hurushwa siku ya Jumapili kila juma kuanzia saa 12:00 -3:00 Asubuhi kimepewa hadhi ya kusimamia usomaji wa magazeti hayo kuanzia saa 1;00 – 1:15 Asubuhi kila Jumapili ya juma.