WASANII WA INJILI WATAKIWA KUTOJIKWEZA


MBEYA
WASANII wa nyimbo za injili nchini wametakiwa kutokujiona wako bora wanapoinuliwa na uimbaji wao na kuanza kujisifu na kujiingiza katika mashindano ya kidunia bali watambuwe kuwa uwezo huo ni kutoka kwa Mungu.
 
Hayo yalisemwa na msanii wa nyimbo za injili Elia Bisangu alipofanya mahojiano kwa simu na mwandishi wa habari hizi  wakati wa kujiandaa na tamasha la uzinduzi wa Albamu ya msanii mwenzake Gerald Sedekia wa Mbeya.
 
Bisangu alisema baadhi ya wasanii wa nyimbo za injili wanapojikuta kuwa nyimbo zao zimekubalika na watu wengi wanajisahau na kuanza kujisifu kuwa wanajua kuimba na kuanza kujiingiza katika mambo ya kudunia jambo ambalo amesema linaanza kupoteza lengo la uimbaji wao.
 
Alisema wao wanapaswa kuangalia nini Mungu alichowapatia wasiangalie manufaa ya kwao wenyewe akidai kuwa iwapo wataangalia ya kwao huwenda Mungu akaamua kuwashusha kwa kuwa neno la Mungu linapaswa litumike ipasavyo kwa misingi ya kimungu.
 
Aliongeza kuwa kwasasa wasanii walioko kwenye chati ya uimbaji kwa nyimbo za injili wamekuwa wakiweka kipaumbele cha kunufaika wao wenyewe badala ya kuendeleza kuhubiri neno la mungu kwa kupitia nyimbo zao.
 
Hata hivyo alisema hata kama wanapohitajika sehemu za kuhubiri neno la Mungu wanatanguliza kwanza maslahi yao mbele ambapo ni gharama kubwa na kuwafanya watu wengine kushindwa kupata mahubiri yao kupitia uimbaji.
 
Kwa upande wake  Gerald alisema kutokana na umuhimu wa ujumbe huo wa Mungu watu pia wanaangalia matendo ya muimbaji mwenyewe kwa hivyo iwapo mtu atabainika kuwa anatanguliza maslahi yake mbele nao watu wanaokuangalia hubadilika na kuanza kukuchukulia kama ni mwimbaji wa nyimbo za kidunia.

Imeandikwa na Michael Mbughi
Imehaririwa na Johnson Jabir

Post a Comment

Previous Post Next Post