Mchungaji wa Kanisa la Moravian Ushirika wa Ruanda Mkoani Mbeya Asafisye Mwangosi amewataka waislam nchini kutoilazimisha serikali kuunda mahakama ya kadhi ili kudumisha mshikamano.
Mwangosi aliyasema hayo hivi karibuni kwa njia ya simu akinukuu katiba ya nchi inayosema Tanzania haina dini rasmi ila watu wake ndio waumini wa dini mbalimbali.
Mchungaji Mwangosi alisema, kitendo cha kunga’nga’nia kuanzishwa kwa mahakama ya kadhi ni kuvunja katiba ya nchi ambayo imeweka misingi ya upendo na mshikamano kati ya waumini wa dini zote.
Alisema kama jambo hili litaachiwa liendelee bila kukemewa na serikali hali hiyo inaweza kuifanya serikali kujiweka mahali pabaya kwa kuwa itakuwa inachangia udini jambo ambalo watanzania hajawahi kuliona tokea uhuru.
Mchungaji Mwangosi amesema ni jukumu la wananchi wote wa Tanzania kuishauri serikali iondokane na mawazo hayo ambayo baadae yanaweza kusababisha kuwagawa watanzania na kuvuruga amani ya nchi.
Mchungaji huyo ameitaka serikali ikemee kwa nguvu zote hoja ya mahakama ya kadhi ili isije ikaondoa umoja na mshikamano uliopo.