JUKWAA LA KIKRISTO LAWAONYA WAISLAMU NA SERIKALI



Wakati dunia ikisheherekea Kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo duniani kote, hapa nchini Tanzania madhehebu ya Kikristo yaliyo chini ya Jukwaa la Kikristo yametoa tamko kali kwa serikali na kwa dini ya Kiislamu.

Tamko hilo limetolewa katika ibada ya Christmass iliyofanyika Kitaifa katika Kanisa Katoliki, Moshi Mjini Mkoani Kilimanjaro mapema leo asubuhi.

Suala la uvumi kwamba nchi ya Tanzania inatawaliwa na idadi kubwa ya wakristo Jukwaa la Kikristo nchini limesema huo ni uongo ambao hautakiwi kufumbiwa macho hata kidogo kwani takwimu zinaonyesha uongozi wa juu wa serikali ya Muungano wa Tanzania unaongozwa na waislamu kwa asilimia 90 wakati visiwani Zanzibar ikiwa ni asilimia 100.

Pia Jukwaa la Kikristo nchini limesema suala la Wakristo  kukojolea Kurani ni la uongo na ambalo limekuwa likifanywa na waislamu wenyewe kwa madhumuni ya kuvuruga amani kwani tukio la Mbagala ni mfano tu Waislamu wameshawahi kufanya na serikali imekuwa ikikaa kimya.

Katika tamko hilo wameitaka serikali na watanzania kwa ujumla wake kutunza hadhi ya baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alijitolea maisha yake kwa ajili ya uhuru na demokrasia ya Taifa la Tanzania.

Hata hivyo Jukwaa la Kikristo limeitaka serikali kutokaa kimya kuhusu watu wanaotaka kusambaratisha umoja, amani,utulivu na mshikamano.

Jukwaa la Kikristo limetoa wito kwa waumini wa dini ya Kiislamu kuanza kujirudi kushikamana na wakristo ili kuendeleza mshikamano wa muda mrefu uliokuwepo tangu kupata uhuru miaka 51 iliyopita.

Aidha Jumapili ijayo ya Desemba 30, 2012 Wakristo nchini watafanya maombi kuiombea nchi kwa mwaka 2013 ili Mwenyezi Mungu aendelee kuweka mkono wake.

Post a Comment

0 Comments