SERIKALI YATAKIWA KUTOKAA KIMYA VISA VYA UCHOCHEZI



Matamko mbalimbali yametolewa wakati huu wa kusherekea sikukuu za mwishoni mwa mwaka ambapo Jukwaa la Kikristo limeitaka Serikali kutokaa kimya katika masuala ambayo yanaweza kuharibu amani ya nchi ya Tanzania.

Jukwaa la Kikristo limesema Serikali imekuwa ikikaa kimya kwa vitendo vyenye kutaka kulichokoza Kanisa la Tanzania kuhusu wakristo kukojolea Kuran, Msahafu wa dini ya Kiislamu. Katika hilo Jukwaa la Kikristo limesema vitendo hivyo vimekuwa vikifanywa na waislamu wenyewe kwa madhumuni ya kutaka kuvuruga amani na mshikamano ambayo nchi imekuwa nayo kwa miaka 51 iliyopita tangu kupata uhuru wake mwaka 1961

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Konde limetoa tamko la kuitaka Serikali kuunda baraza litakalokuwa na uwezo wa kuvichunguza vyombo vya dola vinapokiuka maadili au kushindwa kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Tamko hilo lilitolewa na Askofu wa Dayosisi ya Konde mkoani Mbeya, Dk. Israel Peter Mwakyolile katika Kanisa la Usharika wa Betheli lililopo eneo la Sae jijini Mbeya, wakati wa ibada ya sikukuu ya Krismasi. Amesema KKKT pamoja na Jumuiya nyingine za Kikristo wamekuwa hawaridhishwi na hatua zinazochukuliwa na vyombo vya dola kukemea na kudhibiti matukio mbalimbali yanayoashiria uvunjifu wa amani nchini.

Katika suala la Utoaji mimba  Watanzania wametakiwa kupinga vikali sera ya utoaji wa mimba pamoja na udhibiti wa ongezeko la watu kwani mambo hayo ni kinyume cha mpango wa Mwenyezi Mungu. Kauli hiyo imetolewa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma, Mathias Joseph Issuja, katika ibada ya kusherehekea Sikukuu ya Krismasi, iliyofanyika katika Kanisa la Kiaskofu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba Jimboni Dodoma.

Naye Mchungaji wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Evance Lucas, aliwataka wazazi wenye watoto, ambao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kuhakikisha wanawapeleka shule badala ya kuwaacha majumbani kama walinzi wa nyumba. Mchungaji Lucas alisema wazazi wanatakiwa kutambua kuwa haki ya mtoto ni elimu, hivyo wasiwafanye kama walinzi wa nyumba jambo, ambalo alisema halimpendezi Mungu.

Post a Comment

0 Comments