VIONGOZI mbalimbali wa
Dini wamelaani vikali matukio ya baadhi ya viongozi wa serikali kuvamia maeneo
ya Ibada na kuwashambulia wananchi kwa risasi, na kuiomba serikali kuyavalia
njuga matukio ya aina hiyo.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti huku wakitolea mfano tukio la hivi karibuni ambapo Mkurugenzi
wa halmashauri ya wilaya ya Itigi mkoani Singida Pius Luhende, anadaiwa kuvamia
kanisa la Waadventista(SDA), Wasabato akiwa ameambatana na viongozi wenzake na
kumfyatulia risasi muumini huyo, akiwa ibadani na kusababisha kifo chake.
Akizungumzia tukio
hilo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Victorious la mjini Moshi, mkaoni
Kilimanjaro Dk Sixbert Mkelemi amelaani vikali kitendo hicho na kufafanua kuwa,
eneo la Ibada linapaswa kuheshimiwa na siyo kugeuzwa uwanja wa
vita.
“Sisi viongozi wa dini
tumekuwa tukishirikiana na serikali katika masuala mbalimbali ya kiroho na hata
ya kijamii, na tukio lililotokea mkoani Singida, linalodaiwa kufanywa na
kiongozi wa serikali la kumpiga kijana mdogo kama yule risasi katika eneo la
Ibada na kusababisha kifo chake limetushtua na kutushangaza sana”,
alisema Mkelemi na kuongeza, tunaomba sheria ifuate mkondo wake.
Askofu Dk Mkelemi aliendelea kusema kuwa,
kama muumini huyo alikuwa akisakwa na mamlaka za kiserikali wangemsubiri atoke
Ibadani ama wangetumia njia yoyote ya kumuita badala ya kuvamia Kanisa na
kumfyatulia risasi zilizotoa uhai wake jamabo lililosababisha taharuki kwa
waumini wote Ibadani hapo.
“Viongozi Kupewa madaraka siyo kwenda kuumiza
ama kuwaua watu; hali kama hii ikiendelea amani tunayojivunia kuwa nayo hapa
nchini itatoweka kama vile barafu iyeyukavyo inapopata joto”, alisema.
Makamu Sheikh wa Bakwata Mkoa wa Kilimanjaro
Mlewa Shaban na Katibu wa Bakwata Mkoa wa Kilimanjaro Awadhi Lema, walitoa wito
kwa viongozi wa kiserikali, kuacha kutumia vibaya nafasi zao walizoaminiwa na
Rais Dk John Magufuli.
Aidha viongozi hao wamewataka waumini wa
madhehebu ya Kikristo na yale ya Kiislamu kuwa watulivu wakati vyombo vya
ulinzi na usalama vikiwa vinafanya kazi zake ambapo walitoa rai kwa haki
itendeke katika kushughulikia swala hilo.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa
Kanisa la Furaha Tanzania (KLFT), Jones Molla amelaani kitendo hicho
na kusema kuwa nyumba za Ibada zinapaswa kuheshimiwa.
Naye Askofu mkuu wa Kanisa la
International Christian Centre (KICC) la mjini Moshi, Dk Glorious Shoo,
amelaani kitendo hicho na kuiomba serikali ichukue hatua mara moja dhidi ya
tukio hilo la mauaji ya kutisha tena ndani ya nyumba ya Ibada.
“Natoa ushauri kwa viongozi wakuu waandamizi
turudi tulikotoka kwani awali ilikuwa mtu hapewi nafasi kubwa ya uongozi bila
kupitia mafunzo maalumu ya uongozi kutoka Chuo cha Uongozi Kivukoni; sasa hivi
kuna utofauti kwani kuna viongozi wanapewa madaraka bila kupata elimu ya
maadili ya uongozi”, alisema Dk. Shoo.
Askofu Dk Shoo pia alipendekeza kuwa
watumishi wa Umma wanaopewa ajira wawe ni wale wenye hofu ya Mungu, ambapo pia
alipendekeza kuwepo na semina elekezi ili kuwafunza watumishi wa umma maadili
mema ili kuepuka yale yaliyotokea Singida.
Story
by: Kija Elias
Edited
by: Jabir Johnson
Photograph: Bruxy
0 Comments