Familia ya Mangi Mkuu Thomas Marealle II OBE ya Kilimanjaro
imetoa kitabu cha historia ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini kuanzia mwaka
1902 hadi 1912 kwa kanisa hilo.
Katika tukio hilo Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Dkt. Fredrick Onael Shoo alipokea
vitabu zaidi ya 100 vya historia ya kanisa hilo Afrika Mashariki kutoka kwa
familia ya Mshumbue Marealle II OBE aliyetafsiri kutoka lugha ya kiingereza
hadi Kiswahili.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kumkabidhi iliyofanyika
ofisini kwa Askofu Mkuu Dkt. Shoo hivi karibuni, Themi Marealle ambaye ni miongoni mwa wanafamilia ya Marealle II
alisema wameamua kufanya hivyo ili waumini watakaokisoma waweze kujua historia
yao.
“Kwa hiyo kitabu hiki ni historia ya KKKT hapa Kaskazini na tunaomba kukukabidhi kitabu hiki ili
waumini na hata watu wengine watakaopata nafasi ya kukisoma wajue historia yao,
Baba Askofu nakushukuru sana Mungu akubariki.” alisema Themi Marealle.
Katika hafla hiyo Themi Marealle aliongeza kuwa kitabu hicho
kiliandikwa kwanza na wachungaji wawili wa Kijerumani ambao ni Adolphi na
Shantz.
“Baba Askofu tumefika hapa kukabidhi kitabu chenye historia
ya Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanganyika maeneo ya Kilimanjaro, Arusha, Meru
na Pare; kiliandikwa mara ya kwanza na wachungaji wawili Wajerumani baada ya hapo mheshimiwa Marealle alimwomba
mwalimu wa International School Moshi akitafsiri kutoka kijerumani hadi
kiingereza naye akakitafsiri kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili ili watu wa
Kilimanjaro na Tanzania waweze kukisoma,” aliongeza Themi.
Kwa upande wake Askofu Mkuu Dkt. Shoo alisifu ujasiri huo na
uzalendo wa familia hiyo waliouonyesha kwa kanisa na kwamba ni mfano wa kuigwa.
Aggrey Marealle akisalimiana na Askofu Mkuu Dayosisi ya Kaskazini Dkt. Fredrick Onael Shoo, katikati ni Themi Marealle. |
“Shukrani kwanza kwa familia kwa kupenda kutoa kitabu hiki
ambacho ni kizuri sana kwa historia ya kanisa letu kuanzia mwaka ule wa 1902
hadi 1912 huu ni mchango mkubwa sana ambao Mangi Mkuu Thomas Marealle
ametuachia, lakini familia kipekee ikaona isibaki na vitabu bali wavitoe sadaka
yao kwa kanisa,” alisema Askofu Shoo.
“Napenda kuwashukuru sana kwa sadaka. Ni imani yangu kwamba
vitabu hivi vitatumika kwa kuwapatia watu sio kizazi cha sasa tu lakini hata
vizazi kinachokuja ufahamu wa historia ya uwepo wa kanisa letu la Kiinjili la
Kilutheri hasa katika eneo hili la Kaskazini,” aliongeza Askofu Shoo.
Familia hiyo imetoa kitabu hicho chenye kurasa 207
kinachojulikana, “HISTORI YA KANISA LA
KIINJILI LA KILUTHERI AFRIKA MASHARIKI 1902-1912 (Kilimanjaro, Arusha, Meru
na Pare).”
Mangi Mkuu Thomas Marealle II OBE alitafsiri kitabu hicho
akiwa na msaidizi wake Rusk Shirima Kishimba; ambapo Kitabu hicho kiliandikwa
kwa mara ya kwanza kwa lugha ya Kidachi (Kijerumani). Baada ya hapo
kilitafsiriwa kutoka Udachi hadi kiingereza na Mhisani Anthony Pyane wa London.
CHANZO: JAIZMELA News
ADDITIONS: MCRCTV
Tags
TANZANIA