Desemba 7, 1963 alizaliwa
mtumishi wa Mungu, mchungaji na mwandishi wa vitabu raia wa Nigeria maarufu kwa
jina la Pastor Chris.
Jina lake halisi ni Chris
Oyakhilome ambaye ni mwanzilishi na Rais wa Huduma ya LoveWorld Incorporated
maarufu Ubalozi wa Kristo. Makao yake makuu yapo Lagos nchini Nigeria.
Ni mtoto wa kwanza wa
familia ya Tim Oyakhilome. Mnamo mwaka 1991 Oyakhilome alimuoa Anita
Ebhodaghe ambaye alizaa naye watoto
wawili wa kike.
Mwanamke huyo aliachana na
Pastor kwa kesi iliyopelekwa katika Mahakama moja jijini London mnamo Aprili 9,
2014.
Baada ya kutalikiana
(wadaawa) iliamuliwa mahakamani hapo kuwa watabeba majukumu ya kuwalea watoto
hao wawili.
Talaka ilitoka Oktoba 6,
2016 baada ya miaka 25 ya wawili hao kuishi pamoja huku kiini kikubwa cha
kuachana kwao kikitajwa kuwa ni ‘Tabia zisizovumilika.”
Mnamo Oktoba 6, 2018 binti
yake wa kwanza anayefahamika kwa jina la Sharon aliolewa na raia wa Ghana
Phillip Frimpong katika harusi ambayo inaelezwa kuwa mama yake hakushiriki.
Mnamo mwaka 2011 jarida la
Forbes lilikadiria utajiri wa Oyakhilome kuwa ni kati ya dola za kimarekani
milioni 30 hadi 50.
Katika suala la huduma yake
Pastor Chris amekuwa akifanya kazi katika nchi mbalimbali zikiwamo Uingereza na
Marekani na pia ana vipindi nchini Afrika Kusini na Canada.
Pia Pastor Chris amekuwa
akifanya huduma ya uponyaji katika mikutano yake nchini Ghana.
Pastor Chris amekuwa
miongoni mwa waanzilishi wa kwanza wa kufanya huduma katika vipindi vya
televisheni vinavyoruka toka barani Afrika kwenda ulimwenguni kote.
Mnamo mwaka 2005 aliweka
rekodi ya kukusanya watu katika mkutano wa usiku wa Neno la Mungu, tukio ambalo
lilipewa jina la ‘Good Friday Miracle Night’.
Takribani watu milioni 3.5
walihudhuria. Nchini Afrika Kusini
alishafanya tukio lililopewa jina la Night of Bliss lililofanyika katika Uwanja
wa Mpira wa FNB jijini Johannesburg.
Pastor Chris amekuwa
akifanya huduma yake kupitia mtandao wa Intaneti hususani mitandao ya kijamii
katika nchi tofauti.
Mnamo mwaka 2013 aliweka
rekodi ya kuwa na wafuatiliaji katika mtandao wa Twitter milioni 1.2 pia
milioni 1.9 katika Facebook. Pastor Chris anaendesha mtandao wa kuchati wa
KingsChat.
Katika masuala ya uandishi
wa vitabu ameandika vitabu vingi vikiwamo ‘Rhapsody of Realities’. Kitabu hicho
kimeweka rekodi ya pili duniani kwa kutafsiriwa katika lugha mbalimbali baada
ya Biblia.
Pastor Chris alipata
udaktari wa heshima kutoka katika vyuo vikuu viwili Ambrose Alli na Benson
Idahosa vyote vya nchini Nigeria.
Hata hivyo Pastor Chris
amepitia katika changamoto nyingi katika huduma yake ikiwamo mafundisho yake
kuhusu ndoa.
Alijikuta akipata upinzani
mkali kutoka katika mitandao ya kijamii kuhusu usawa katika ndoa kwa mtazamo
wake wa kidini.
Katika mojawapo ya chapisho
lake katika ukurasa wa Facebook lililopewa jina la ‘Who is a Husband and What is his role?’ lilileta
ukosoaji mkali ambapo katika ndani yake ilionyesha wanaume ni ‘Masters’.
Katika hilo Pastor Chris alisema matatizo
mengi katika ndoa za Kikristo yanatokana na Mungu mwenyewe kutoweka wazi maana
halisi ya kuolewa.
Pastor Chris alisema wanawake
wanaamini kuwa wapo sawa katika mapenzi lakini kuwa na mume haimanishi kuwa ni
mpenzi wake bali ina maana ya mkuu yaani Master.
Alikaririwa akisema, “
Biblia inasema mwanaume ni kichwa cha mwanamke (1 Kor. 11:3) kwa hiyo
unapoolewa unaingia katika mamlaka yake. Na sio kwamba mtakuwa sawa katika
mamlaka, licha ya kwanza ninyi nyote wawili ni warithi wa Ufalme wa Mungu.”
Pia Pastor Chris alipata
upinzani mkali kuhusu mtazamo wake wa kidini kwenye mapambano dhidi ya
VVU/UKIMWI kwa kile alichosema maradhi kama hayo yanaweza kutoweka kwa kukemea
kwa Jina la Yesu.
Tags
HAPPY BIRTHDAY